Kulingana na gazeti la Mwananchi la tarehe 11/02, Wabunge wawili, mmoja wa CCM na mwingine wa Chadema, jana walikula vichapo walipokuwa katika harakati za uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika katika kata 27 nchini.
Wabunge hao, Godbless Lema (Chadema) wa Arusha na Mchungaji Jackson Mwanjele wa Mbeya Vijijini walipata vipigo katika matukio tofauti yanayohusiana na uchaguzi huo.
Lema alidai kuwa alinusurika kifo kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa polisi na ilibidi aanguke chini na kujifanya amezirai ili kujiokoa, katika tukio lililotokea jana jioni, eneo la Shule ya Sombetini alipokuwa akielekea katika kituo cha kupigia kura.
Mara baada ya kufika jirani na kituo cha Sombetini, inadaiwa kuwa polisi walisimamisha gari ya Lema na kuanza kumuhoji lakini ghafla ilitokea kutoelewana kipigo kuanza. Katika tukio hilo, Lema alipata kipigo hadi kuangukia katika mfereji na akiwa chini, alionekana kama amezimia hivyo polisi walimuachia na kuokolewa na wafuasi wa Chadema.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Lema alisema bila kujifanya amezirai angeweza kuuawa... “Wamenipiga sijui kosa langu, mimi kama mbunge niliitwa na mawakala wakiomba gari kubeba masanduku na ni kweli nilikuwa nimewasha taa za gari nikishangilia. Kesho naenda kupimwa hospitali kwani nina maumivu kwenye mbavu. Baada ya hapo nitajua cha kufanya kwani walionipiga nawajua.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana jana kuelezea tukio hilo lakini mmoja wa polisi waliokuwa eneo la vurugu hizo, alisema walilazimika kimdhibiti Lema, kwani alikuwa anafanya fujo jirani na kituo cha kura.
“Hakuna aliyempiga, alianguka mwenyewe kwenye mfereji, tulimtaka aondoke kwa amani akagoma,” alisema askari huyo.
No comments:
Post a Comment